Kwa mujibu wa mwandishi wa habari wa Shirika la Habari la Hawza kutoka Mashhad, Anwar al-Tawil, mwenye shahada ya uzamivu katika Sheria kutoka Chuo Kikuu cha Mansoura nchini Misri na mwanaharakati wa Palestina, siku ya Alhamisi, tarehe 26 Shahrivar (Sep 17 2026), katika kikao cha pili cha kielimu kilicholenga Mhimili wa Muqawama, umoja na mshikamano wa Umma wa Kiislamu dhidi ya mfumo wa kibeberu unaozingatia mafundisho ya Ridha na fikra za kiongozi shahidi, kilichofanyika pembezoni mwa kikao maalumu cha Kongamano la Kimataifa la Imam Ridha (as) katika ukumbi wa Sheikh Tusi, huku akieleza vipengele vya kisheria na kibinadamu vya migogoro ya eneo hilo, alisema: “Utafiti uliofanywa umechunguza maeneo makuu matatu: mgogoro wa maji katika Asia Magharibi, hali ya Ukanda wa Ghaza na mgogoro wa nishati katika nchi za Kiarabu na Kiislamu.”
Akizungumzia mhimili wa kwanza wa utafiti huo, alihusisha mgogoro wa maji katika Asia Magharibi na uthabiti wa eneo hilo pamoja na suala la utawala wa kimataifa, na kuongeza: “Upungufu wa maji katika eneo hili si suala la kimaumbile pekee, bali namna ya kugawa rasilimali, usimamizi wake na nafasi ya madola yenye kutawala katika jambo hili vina umuhimu wa msingi.”
Uzoefu wa Mwanaharakati wa Palestina wa Miezi Sita ya Vita vya Ghaza
Al-Tawil aliendelea kwa kurejelea uzoefu wake binafsi wa kuwepo Ghaza katika miezi ya mwanzo ya vita, akisema: “Mwanzoni mwa vita nilikuwa katika Ukanda wa Ghaza na nilikaa takribani miezi sita katika kipindi cha vita kali zaidi. Katika kipindi hicho, hakuna mkazi yeyote wa Ghaza aliyekuwa na usalama wa maisha yake, na watu kila wakati walikuwa wakihofia uwezekano wa kuuawa wao pamoja na familia zao.”
Aliongeza: “Ukali wa mashambulizi ulifikia kiwango ambacho mitaa ilikuwa ikilengwa mabomu, na wakati mwingine majengo kadhaa yalibomolewa kwa wakati mmoja. Nyumba yangu ilikuwa katika ghorofa ya nane, na kwa macho yangu nilishuhudia majengo yakiharibiwa na kuanguka juu ya wakazi wake.”
Mwanaharakati huyo wa Palestina aliendelea: “Katika baadhi ya mashambulizi, mamia ya watu walipoteza maisha yao kwa wakati mmoja, na familia ziliangamizwa kabisa na majina yao kufutwa katika sajili ya raia.”
Nguzo Tatu Muhimu za Maisha ya Watu wa Ghaza Zimekumbwa na Mgogoro
Al-Tawil, akieleza kwamba, mgogoro wa Ghaza hauishii tu katika upungufu wa chakula, alifafanua: “Maji, chakula na nishati ni nguzo tatu muhimu za maisha ya mwanadamu, na huko Ghaza nguzo zote tatu zimekumbwa na mgogoro mkubwa.”
Alisema: “Tangu siku za mwanzo kabisa za vita, umeme ulikatika kabisa katika Ukanda wa Ghaza, na watu wakaanza kutumia paneli za sola, betri na jenereta ili kupata nishati; lakini baada ya mafuta kukatwa, jenereta nazo zilisimama kufanya kazi.”
Aliendelea: “Hata paneli za sola zililengwa katika mashambulizi, na katika baadhi ya matukio nyumba, vifaa vya nishati na wakazi wake walijeruhiwa au kuathiriwa kwa wakati mmoja.”
Mwanaharakati huyo wa Palestina, akirejelea hali ngumu ya upatikanaji wa chakula huko Ghaza, alisema: “Katika kipindi fulani, bei ya mfuko mmoja wa unga wenye uzito wa kilogramu 25 ilifikia takribani dola 500 hadi 600, na familia zililazimika kugawana mkate mmoja miongoni mwa wanafamilia.”
Rasilimali za Asili Zinapaswa Kuwa Katika Matumizi ya Wanadamu Wote
Al-Tawil, katika sehemu nyingine ya hotuba yake, akirejelea aya za Qur’ani Tukufu kuhusu maji, kilimo na moto, alisema: “Qur’ani Tukufu inapozungumzia maji na chanzo chake, inamuelekeza mwanadamu kutambua uwezo na uumbaji wa Mwenyezi Mungu, na jambo hili linaonesha kuwa; rasilimali muhimu za maisha kama maji haziwezi
kufafanuliwa katika mfumo wa umiliki na utawala wa mtu binafsi.”
Alisisitiza: “Rasilimali hizi zimerahisishwa kwa ajili ya wanadamu wote, na si mali maalumu ya Waislamu pekee, kwa hiyo, kunufaika na rasilimali muhimu za maisha kunapaswa kuzingatiwa kwa mtazamo wa kibinadamu na unaozingatia uadilifu.”
Al-Tawil pia, akirejelea riwaya isemayo: «الناس شرکاء فی ثلاث، الماء والکلأ والنار», alisema: “Kuhusu maana na tafsiri ya riwaya hii, kuna mitazamo mbalimbali, na mimi sijioni kuwa mtaalamu katika jambo hili; hivyo uchunguzi wa kina wa suala hili nawaachia wanazuoni na wataalamu, hata hivyo, riwaya hii pamoja na aya za Qur’ani vinaweza kutoa msingi wa mjadala kuhusu rasilimali za umma na umuhimu wa kuzuia rasilimali hizo kuwa chini ya ukiritimba.”
Akizungumzia suala la uadilifu katika ugawaji wa utajiri wa umma, aliongeza: “Serikali ya Kiislamu inapaswa, kupitia usimamizi sahihi na makini, kuweka mazingira ya kuwawezesha watu kunufaika kwa usawa na utajiri wa umma, ili kuzuia ubaguzi na kupotezwa haki.”
Mgogoro wa Maji katika Asia Magharibi Sio Suala la Upungufu wa Rasilimali Pekee
Al-Tawil aliendelea kuzungumzia mgogoro wa maji katika Asia Magharibi, akisema: “Mgogoro wa maji katika eneo la Asia Magharibi na eneo linaloitwa Mashariki ya Kati ni suala lililo wazi; lakini tatizo si upungufu wa maji pekee, bali namna ya kugawa rasilimali na uingiliaji wa madola yenye kutawala katika usimamizi wa rasilimali hizo pia una umuhimu.”
Alirejelea baadhi ya masuala ya maji katika nchi za eneo hilo, akisema: “Suala la mito nchini Afghanistan, suala la Bwawa la Al-Nahda nchini Misri, hali ya mito ya Tigris na Euphrates na uhusiano wa maji kati ya Uturuki na Iraq, pamoja na masuala yanayohusiana na maji kati ya Iran na Afghanistan, ni miongoni mwa masuala yanayopaswa kuchunguzwa katika mfumo wa mahusiano ya kikanda.”
Akizungumzia hali ya Iran, aliongeza: “Upungufu wa maji ndani ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia ni suala kubwa, na shinikizo la kiuchumi pamoja na vikwazo zinaweza kuongeza matatizo na shinikizo lililopo katika sekta ya maji na nishati.”
Mgogoro wa Nishati; Suala la Kimkakati Katika Haki za Mataifa
Mwanaharakati huyo wa Palestina aliendelea kwa kurejelea mgogoro wa nishati, akisema: “Katika nyaraka nyingi za kisheria na mikataba ya kimataifa, haki ya mwanadamu kupata chakula imejadiliwa, lakini haki ya mwanadamu kupata nishati imepewa umuhimu mdogo; ilhali nishati ni miongoni mwa masuala ya kimkakati na msingi katika maisha ya mwanadamu wa leo.”
Al-Tawil aliongeza: “Mlango wa Hormuz na Bab al-Mandab vinaonesha kwamba, nishati si suala la kiuchumi pekee, bali linahusiana moja kwa moja na usalama wa kikanda na mahusiano ya kimataifa.”
Pia alizungumzia suala la matumizi ya amani ya nishati ya nyuklia na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, akisema: “Haki ya kutumia nishati ya nyuklia kwa madhumuni ya amani inapaswa kuchunguzwa katika mfumo wa haki za mataifa, na haki hii haipaswi kutekelezwa kwa ubaguzi baina ya nchi.”
Umuhimu wa Kukabiliana na Ubaguzi Katika Kunufaika na Rasilimali
Al-Tawil, akikosoa kile alichokiita viwango viwili katika suala la haki za binadamu, alisema: “Tunapozungumzia haki za mwanadamu na uhuru wa mataifa, misingi hii inapaswa pia kuheshimiwa kwa vitendo kwa mataifa yote, na kunufaika na rasilimali pamoja na teknolojia za kimkakati hakupaswi kutegemea ubaguzi baina ya nchi.”
Akirejelea baadhi ya dhana zilizotajwa katika Qur’ani Tukufu kuhusu ujinga wa zama za Jahiliyyah, alisisitiza umuhimu wa kuzingatia uadilifu na kuzuia ubaguzi, akisema: “Kigezo cha haki za kibinadamu kinapaswa kuwa sawa kwa wanadamu wote. Haiwezekani kuzungumzia haki za binadamu, lakini kwa vitendo tukapuuza haki za baadhi ya mataifa.”
Al-Tawil alisisitiza umuhimu wa kuzingatia mafundisho ya Qur’ani Tukufu, maarifa ya Kiislamu na misingi ya uadilifu katika kukabiliana na migogoro ya kikanda na kimataifa.
Maoni yako